Showing posts with label SIASA. Show all posts
Showing posts with label SIASA. Show all posts

LESENI ZA MAFUTA NA GESI ZAPINGWA NA MNYIKA


WAZIRI Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, amemtaka Rais Jakaya Kikwete kusitisha mzunguko wa nne wa utoaji wa leseni za utafutaji wa gesi asili na mafuta hadi sera na sheria ya gesi asili zikamilike, na marekebisho ya sera ya nishati na sheria za mafuta yafanyike. 

Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo (CHADEMA), alisema hatua hiyo ni kurejea maoni na mapendekezo aliyoyawasilisha bungeni kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Mei 22 mwaka huu.
 
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, alisema rais anapaswa kuchukua hatua hiyo kwa kuzingatia kwamba Mei 25 mwaka huu, badala ya kushughulikia mapendekezo hayo, Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo alitoa majibu ya uongo na upotoshaji bungeni kuhusu masuala mbalimbali.
 
“Aidha Ikulu inapaswa kueleza iwapo Baraza la Mawaziri chini ya Rais Kikwete ndilo lililofanya uamuzi wa kuendelea na mchakato wa kutoa leseni za vitalu vya utafutaji wa gesi asili bila ya kuwepo kwa sera ya gesi asili na sheria ya gesi asili, na sera ya nishati na sheria zinazohusu mafuta au ni maamuzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) na Wizara ya Nishati na Madini,” alisema.
 
Mnyika aliongeza kuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda anapaswa kueleza iwapo kauli ya kejeli, dharau na uongo ya hivi karibuni iliyotolewa na Waziri Muhongo, kwamba uwezo wa wafanyabiashara wa Tanzania ni kuwekeza kwenye soda na juisi, si kwenye sekta ya gesi, ni msimamo wa serikali au maoni ya waziri binafsi.
 
“Izingatiwe kwamba Wizara ya Nishati na Madini, kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), imetangaza mzunguko wa nne wa utoaji leseni za utafiti wa gesi asili na mafuta katika vitalu nane ndani na nje ya maji ya Ziwa Tanganyika vyenye ukubwa wa kilomita za mraba elfu tatu kila kimoja utakaofanyika Oktoba 2013.
  
“Serikali pia imetenga mipaka ya vitalu viwili kwenye bahari kuu, na kuingia ubia wa utafiti na kampuni inayoitwa mbia wa kimkakati (Strategic Partner) ambae serikali haijamtaja,” alisema.
 
Alisema mchakato huu unafanyika wakati taifa likiwa halina sera (mchakato wa kuiandika bado unaendelea) na hatimaye yaanze maandalizi ya kupata sheria mahususi za kusimamia sekta ndogo ya gesi, hatua ambayo inapaswa kuambatana na marekebisho ya kisera na kisheria ya sekta.
 
Aliongeza kuwa tayari Tanzania imeshafanya ugunduzi wa futi za ujazo zaidi ya trilioni 32 za gesi katika maeneo kadhaa nchini, hivyo kuifanya kuwa kati ya nchi vinara wa gesi nyingi Afrika na duniani.
 
“Utajiri huu wa gesi hadi sasa hauna sera wala sheria zinazotoa mwongozo wa usimamizi na udhibiti wake, ili kuhakikisha unawanufaisha Watanzania, kuepuka makosa yaliyofanyika katika uwekezaji mwingine wa gesi asili na rasilimali nyingine uliofanyika bila mifumo thabiti,” alisema.

IDD AMINI APIGWA CHINI MEDALI ZA HESHIMA KWA MARAIS WALIOWAHI KUIONGOZA UGANDA


Idd Amin Dada.

Mwenyekiti wa kamati ya Taifa ya Tuzo na Medali nchini Uganda Jenerali Elly Tumwine ameweka wazi kuwa katika tuzo za heshima zilizotolewa kwa marais waliowahi kuingoza nchi hiyo pamoja na watu wengine ambao mchango wao unatambulika..

 Aliyewahi kuwa rais nchini humo Hayati Field Marshal Idi Amin Dada hakupata heshima kwa sababu aliacha urithi wa mfumo mbaya wakati wa uongozi wake.

Marais wote wametunukiwa Medali za Miaka 50 ya Uhuru wa Uganda wakati wa maadhimisho ya sherehe za chama cha NRM kutimiza miaka 27 yaliyofanyika wilaya Kasese, ambapo rais Yoweri Museveni alipokea medali ya, sambamba na watu wengine 43.
Jumla ya watu 3,500 nchini Uganda watapokea tuzo hiyo ambayo inawatambua mtu mmoja mmoja kwa mchango wake katika kutoa huduma na uzalendo kwa nchi hiyo tangu ilipopata uhuru.

Jenerali Tumwine amesema Amini hakutambuliwa kwa sababu ya mfumo mbaya alioutumia wakati wa uomgozi wake.

Amini alikuwa rais wa Uganda kutoka mwaka 1971 hadi 1979 ambapo aliingia madarakani kwa kupindua serikali ya Milton Obote Januari 1971.

Marais wengine wote waliopita wakiwemo Sir Edward Mutesa, Obote, Yusuf Lule, Godfrey Lukongwa Binaisa na Gen. Tito Okello, wametunukiwa medali hizo za heshima.

BALOZI SEIF AWAJULIA HALI MAJERUHI WA JAHAZI LILILOZAMA ZANZIBAR


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimfariji Abiria Juma Ali Jaku wa Jahazi ya Sun Rise iliyopata ajali na kuzama  kati ya Tanga na Mkokotoni ikiwa imebeba Abiria 32 kati ya hao 21 wameokolewa na saba hadi sasa hawajapatikana. Kushoto ya Balozi Seif ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mh. Pemba Juma Khamis.

Nahodha wa Jahazi ya Sun Rise iliyozama kati ya Tanga na Mkokotoni Bwana Abdulla Saleh akimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mkasa uliowapata wa kuzama baada ya chombo chao kupatwa na dhoruba kali.

WAFANYAKAZI WA SERIKALI GAMBIA SASA KUFANYA KAZI KWA SIKU 4 TU KWA WIKI KWA MSHAHARA ULE ULE



Serikali ya Gambia imetambulisha mfumo mpya wa siku za kufanya kazi kwa wafanyakazi wa serikali ambapo sasa watafanyakazi kwa siku nne tu, huku siku ya Ijumaa nayo ikiwa siku ya mapumziko.

Rais wa nchi hiyo Yahya Jammeh (pichani) amesema wananchi wa Gambia ambao wengi wao ni waislamu sasa watapata muda zaidi kusali, kushiriki shughuli za kijamii na kulima mashamba yao.

Kwa mujibu wa taarifa ni kuwa sasa wananchi wa Gambia wanapaswa kuingia mashambani kupanda mazao ya chakula na kutumia chakula hicho ili taifa hilo liwe tajiri.

Rais huyo amesema mishahara haitapunguzwa kwa sababu kwa siku hizo nne watu watafanyakazi zaidi ya saa za kawaida ili kufidia siku ya tano.

Shule za serikali sasa hazitafunguliwa tena Ijumaa, ila sekta binafsi zitafanyakazi zao ila hazitaweza kufanya biashara yeyote na serikali siku hiyo.

Rais Jammeh mwenye historia ya kuwa na tabia za kustaajabisha hajawapa wananchi wa Gambia muda wa kujiandaa kwa mfumo huo mpya.

Rais Jammeh aliingia madarakani kwa mapinduzi yaliyomwaga damu mwaka 1994.


 
Support : mpekuzi | John mpekuzi | Wataalam
Copyright © 2009. DODOSO - All Rights Reserved
Template designed by mpekuzi
Proudly powered by Blogger