Tunajua
wote kwamba, hutokea wanawake wakateswa sana kwenye uhusiano wao wa
kindoa au kimapenzi na bado wakaendelea kukaa tu kwenye uhusiano huo.
Inafikia hadi mtu anakufa huku akiona kabisa. Watu wengine huiita hali
hii kuwa ni ujinga na wengine huita kulogwa au huelezea hali hii kwa
njia ambayo haiwapi haki wanawake hao. Zipo sababu nyingi ambazo
zinawafanya wanawake kuendelea kukaa kwenye ndoa ngumu, bila hata
kufikiria kuondoka. Sababu nyingine zinaweza kuonekana kama kituko,
lakini ndizo zinazowafanya wafie kwenye ndoa.
Kuna
ile sababu kwamba, hawajui ukubwa wa kiwango cha mateso. Hii hutokana
na kwamba, baada ya kuzoea mateso, mwanamke hufikia kuamini kwamba, hayo
siyo mateso, bali ndivyo ndoa inavyotakiwa iwe. Kuna sababu ya kukosa
marafiki, ndugu au jamaa wa karibu. Na kwa sababu hana watu wa aina
hiyo, inakuwa vigumu kwake kuwa na mahali pa kukimbilia ili aweze kupata
nafasi ya kujiandaa kuanza upya maisha.
Kuna
wanaoendelea kukaa kwa sababu dini zao zinawaambia, hawana budi kukaa,
kwani wameshakuwa mwili mmoja na waume zao na hivyo hawawezi kuondoka.
Wanafikiria iwapo wataamua kutoroka, viongozi wao wa dini watawaona vipi
na waumini wenzao watachukuliaje jambo hilo. Kwa hiyo, wanaishi kwenye
ndoa hizo kwa sababu ya dini, siyo kwa sababu yao binafsi. Halafu kuna
suala la kupenda. Utegemezi wa kihisia huwa unaitwa kupenda. Kwa hiyo
mwanamke anasema anampenda fulani kiasi kwamba, hawezi kumwacha, wakati
ukweli ni kwamba, anamtegemea mwanaume huyo kihisia.Wanawake wanaoteswa
kwenye ndoa, huwa wanajidanganya kwamba, watamudu siku moja kubadili
tabia hiyo a waume zao kuwafuja. Wanajiambia kwamba, kutukanwa, kupigwa,
kudhalilishwa, na matendo mengine, siyo hiari ya hao waume wao.
Hivyo
wanaamini kwamba, kuna siku watamudu kuwasaidia watoke kwenye tabia
hizo. Lakini wakati mwingine wanaume hawa watesaji, huwa wanajidai
kusema kwamba, wanafanya mambo hayo bila kujua sababu na kuna wakati
wanasema wamelogwa.Hujawahi kuwaona wanawake wanaokwenda kwa waganga
kutafuta dawa ili waume zao wasiwapige, ati kwa sababu vipigo vyao
vinatokana na kuchananywa na uchawi wanaofanyiwa na wanawake zao wa nje?
Mwanamke anaamini kabisa kwamba, mumewe hamjali na anamdhalilisha kwa
sababu ya kulogwa!Mwanamke anaweza kujiambia kwamba, kwa sababu mume
wake kuna wakati anamtendea wema, hata kama ni moja, basi anampenda na
hayo mengine mabaya, yatakwisha au ni bahati mbaya.
Mwanamke
pia anaweza kufikiri kwamba, akijitahidi sana kumfurahisha mumewe, mume
huyo atabadilka na kuwa na tabia nzuri. Hivyo hujipendekeza na mwanaume
habadiliki na mateso yanaongezeka. Kuna wanaomudu kuishi kwenye
uhusiano huu wa sababu, wamemudu kukandamiza, kupunguza ukubwa wa
maumivu. Wanajiambia kwamba, wanavyotendewa siyo vibaya sana. Mwanamke
anaweza kujiambia, ‘alinipiga kidogo tu, tena mara mbili kwa mwezi, kuna wanaopigwa kila siku.’ Huyu amehalalisha kipigo na mateso, hawezi kuondoka.
Kuna
wanawake wanaoamini kwamba, ndoa inajengwa na kuimarishwa na mwanamke
au kuvunjwa na mwanamke pia. Kuna andiko moja katika Biblia hutumiwa
sana kuwatisha, linalosema, ‘Mwanamke m.p.u.m.b.a.v.u huivunja ndoa yake kwa mikono yake mwenyewe.’ Kwa
hiyo wanapofikiria kuondoka, hufikiria kwamba, watu watajua na kumzonga
au kumdharau kwa sababu ameshindwa kulinda ndoa. Wengine ni woga tu,
kwamba, wakiondoka waume zao watawalipizia visasi au watawasumbua. kuna
wakati waume wenyewe ndiyo wanaokuwa wamewatisha kwa kiwango hicho.
KAMA UMEGUSWA NA HUDUMA ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.