Kumekuwa
na maswali yasiyo na majibu miongoni mwa jamii kwamba imekuaje vijana
wa kiume wamekuwa ni waongo sana hasa linapokuja swala la kuoa? Kwa
kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo ambavyo idadi ya wanaume
wanaoogopa kuoa inazidi kuongezeka. Utakuta wapenzi wanaambiana kwamba
wanapendana na kuahidiana kuwa wataoana, lakini kitakachotokea baada ya
hapo ni mwanaume kuanza kupiga chenga kwa visingizio lukuki.
Kwa nini hali hiyo hutokea?
Ukweli ni kwamba hakuna jibu la moja kwa moja juu ya tatizo hilo, lakini yapo mambo ambayo yanaweza kutupa angalau tafakuri. Nitajaribu kudadavua baadhi ya sababu zinazowafanya wanaume siku hizi kukwepa kuingia katika taasisi ya ndoa:
1 Ukosefu wa mtu wa kumchukulia kama mfano: Hapa
nawazungumzia wale watoto wa kiume waliolelewa malezi ya upande mmoja
yaani walilelewa na mama peke yao. Sina maana ya kudharau au kutweza
malezi ya mama, la hasha, lakini ni vyema mkafahamu kwamba kuwa na baba
asiye na malezi mazuri si sawa na kutokuwa na baba. Na ndio maana
nikasema ukosefu wa mtu wa kumchukulia kama mfano. Achilia mbali aina ya
malezi atakayoyapata kwa familia yawe mazuri au mabaya lakini lazima
kutakuwa na tabia za kiume zitakazoakisi malezi ya mtoto wa kiume katika
familia husika. Watoto waliolelewa na mama peke yao kuna kitu huwa
wanakosa, kwani wanakuwa hawana mtu wa kumchukulia kama mfano kwa upande
wa jinsia ya kiume na hapo ndipo hujikuta wakijifunza wenyewe namna ya
kuongea na kutenda kama wanaume kwa sababu katika makuzi yao hawakupata
fursa ya kuwa karibu na baba zao. Kwa kuwa siku hizi kuna kundi kubwa la
kina mama ambao wamejikuta wakiachiwa mzigo wa malezi ya watoto, baada
ya aidha kuachwa na waume zao au kuzalishwa na kutelekezwa (Single
mothers), na hapo ndipo tunaposhuhudia mtoto wa kiume anapokua kwa umri
na kimo huku akiwa hana mtu wa kumuangalia kama mfano wa mume
anavyotakiwa kuwa katika familia zaidi ya kujifunza mambo hayo kupitia
katika TV, senema au miziki. Wanaume waliopitia malezi ya aina hii
huchelewa sana kuoa kwani huyaangalia maisha ya ndoa kwa namna ya
kujaribu na ndipo hapo wengi huishia kuishi kinyumba na wanawake kwa
ajili ya kutaka kujifunza namna ya maisha ya ndoa yanavyotakiwa kuwa na
ndio sababu huchukua muda mrefu kufanya maamuzi. Na mara nyingi huishia
kubadilisha wanawake kutokana na kutokuwa na uhakika wa kile
wanachokitafuta.
2 Mgogoro wa kiuchumi: Kuna
kundi kubwa la vijana siku hizi hawana ajira au hawana uhakika na
kipato. Ukweli ni kwamba hakuna mwanaume atakayependa kujiingiza kwenye
ndoa wakati hana kazi au hana uhakika na kipato chake. Na hiyo ni
kutokana na wanawake wengi siku hizi kuonekana kujali zaidi wanaume
wenye uhakika na kipato. Hii misemo ya wanawake ya kebehi dhidi ya
wanaume wasio na ajira au kipato, kama vile “mwanaume suruale” ina mchango mkubwa sana katika kuwafanya wanaume kukwepa kuoa iwapo hawana ajira au hawana uhakika na kipato chao.
3 Wanawake wengi kuwa na kiwango cha elimu ya juu: Siku
hizi wanawake wengi wameibuka katika kutafuta elimu ya juu kwa juhudi
kubwa. Idadi ya wanawake wanaojiunga na vyuo vikuu ni wengi tofauti na
ilivyokuwa zamani. Na hiyo ni kutokana na wazazi wengi kubadili mtazamo
wao juu ya mtoto wa kike. Zamani mtoto wa kike alichukuliwa kama kitega
uchumi. Kwa maeneo ya vijijini na katika familia masikini, watoto wa
kike walikuwa wanatazamwa kama, ‘biashara ya kesho’ ambapo
watauzwa kwa njia ya mahari. Kwa hiyo thamani yao ilikuwa ni kuolewa,
ni ile ya kibidhaa na sio kibinadamu. Lakini tofauti na zamani siku hizi
hata kule vijijini kumekuwa na mwamko mkubwa sana wa kumsomesha mtoto
wa kike hadi elimu ya juu. Kutokana na mwamko huo wanawake wengi
wamejikuta wakiona elimu kama kimbilio pekee la kuepukana na mfumo dume.
Mwanamke gani atakubali kunyanyaswa na mwanaume akiwa na elimu yake na
labda pia akiwa na kazi yake yenye mshahara na marupurupu ya kutosha,
naamini watakuwa ni wachache sana ambao hawajiamini au waliathiriwa na
malezi. Kwa upande wa wanaume nao, wamejikuta wakiwaogopa wanawake hawa
wenye elimu ya juu kwa hofu ya kuzidiwa kipato na labda kukosa sauti
kama mwanaume na hiyo inatokana na ego tu.
4 Wanaume huwaona wanawake kama tishio wanapokuwa na mafanikio makubwa kifedha: Inaweza
kutokea mwanaume anaweza kuwa na uhusiano na mwanamke ambaye labda tu
nisema ni mbangaizaji. Wakati huo anaweza kuahidi kufunga ndoa na
mwanamke huyo, lakini iwapo itatokea mwanamke huyo akapata mafanikio
kibiashara na kuinuka kifedha. Kama mwanamke asipokuwa makini anaweza
kusababisha mwanaume huyo akaingia mitini. Sababu kubwa hapo inaweza
kuwa ni hofu ya kuogopa kuongozwa na mwanamke. Kumbuka kwamba mfumo dume
bado umetawala vichwani mwa wanaume wengi kutokana na malezi. Mwanaume
asiyejiamini ni vigumu sana kwake kuoa mwanamke aliyemzidi kipato. Kwa
sababu akifanyiwa jambo dogo tu, inakuwa kama ametoneshwa. Atahisi
kutaka kutawaliwa na mwanamke huyo. Jambo ambalo wanawake wanatakiwa
kulifahamu ni kwamba kila mwanaume anataka kutambuliwa na kuheshimiwa
kama shujaa kabla ya kumfuata msichana. Iwapo utakuwa umesimama iwe ni
kifedha au kielimu pale unapotafuta kupata mwenza, inabidi ujishushe
sana la sivyo utadoda.
5 Wanaume wengi siku hizi wana hofu ya majukumu, hasa ya kulea watoto:
Kutokana na malezi yao au kile wanachokijua kuhusu watoto, baadhi ya
vijana huamini kwamba, kulea watoto ni jambo gumu sana. Lakini wengine
wanaamini kwamba, hata mke anapaswa kulelewa kama ilivyo kwa mtoto.
Hivyo wanaamua kutafuta kwanza uwezo ambao haupatikani kiurahisi. Kuna
wengine, ambao wamefundishwa au kuelekezwa na mila na desturi zao
kwamba, kabla hawajaoa, ni lazima wawe na nyumba kwanza, tena kwao. Kwa
hiyo, hawa hadi waje wapate uwezo wa fedha wanakuwa wameshachelewa.
6 Kuna baadhi ya wanaume, maisha bila ya ndoa wanayaona kuwa ndiyo bora kuliko yale ya ndoa: Kuna
baadhi ya wanawake hujirahisisha sana kwa wanaume. Siku hizi ni jambo
la kawaida sana kukuta mwanaume anaishi na mwanamke bila ndoa, wenyewe
wanaita Trial Marriage.
Na hapo ndipo unapokuta wanaume hawaoni tena umuhimu wa kuoa. Sasa kama
mwanamke anaweza tu kuishi na mwanaume bila ya ndoa na mwanaume huyo
akapata huduma zote kutoka kwa mwanamke huyo, unadhani ni kitu gani
kitamvuta kufunga ndoa. Jambo lingine ni ile dhana kwamba maana ya ndoa
ni tendo la ndoa. Siku hizi wanaume wengi wamejikuta wakiwa hawahitaji
tena kuoa kwa sababu tendo hilo linapatikana kiurahisi tofauti na
zamani. Siku hizi inawezekana kabisa kumtongoza binti leo na kupata
tendo siku hiyo hiyo….. Na hapa siwazungumzii makahaba. Nawazungumzia
mabinti zetu ambao wengine ukiwaona ni watu wa kuheshimiwa ukiwaangalia
kwa nje lakini kwa ndani hawana lolote, vijana wa siku hizi wenyewe
huwaita maharage ya Mbeya.
Kuna sababu nyingi zinazotajwa kusababisha wanaume siku hizi kujivuta sana katika kufanya maamuzi ya kutafuta mwenza. Lakini hizo chache nilizozitaja zina mchango mkubwa.
Kuna sababu nyingi zinazotajwa kusababisha wanaume siku hizi kujivuta sana katika kufanya maamuzi ya kutafuta mwenza. Lakini hizo chache nilizozitaja zina mchango mkubwa.
KAMA UMEGUSWA NA HUDUMA ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.