Siyo kila dalili ya mwanaume kupenda ni ya kweli…!
Kuna
wakati ambapo, wanawake wanajikuta wakikabiliwa na swali la, je,
mwanaume huyu ananipenda kweli? Hii hutokea pale anapokutana na mwanaume
ambaye, huenda amevutiwa naye. Pengine mwanaume naye anaweza kuonesha
kuvutiwa na mwanamke huyo.
Kwa hiyo, mwanamke hujiuliza kama akubali ombi la mwanaume huyo na
kukubali kuzungumza naye au kuanzisha naye uhusiano, kama mwanaume
atakuwa amezungumza naye kuhusu jambo hilo. ni kweli kwamba, kuna ugumu
kwa mwanamke kujua hasa ni kwa namna gani anaweza kujua kwamba, huyo
mwanaume amempenda kweli au hapana.
Kuna vitu vingi ambavyo vinaweza kuwa ni dalili ya kumpenda mwanamke, lakini wakati huo huo vinaweza visiwe.
1. Hebu tuchukulie kwamba, mwanaume ameonesha kuwa na tabia tunazoziita
nzuri. Labda amekumbuka kirahisi jina la mwanamke, ameonesha kuwa
msikilizaji mzuri, ameonesha kuwa anajali kuhusu kinachosemwa na
mwanamke, na amekuwa anamuuliza maswali kwa dhati na utulivu. Hapa
mwanamke anaweza kuamini kwamba, huyu mwanaume anampenda. Lakini ukweli
huenda ukawa ni kinyume chake. Inawezekana huyo mwanaume ni muungwana
tu, na anaonesha tabia hizo kutokana na uungwana wake na siyo kutokana
na kumpenda kimapenzi mwanamke.
2. Kuna watu ambao wana upendo, wamekomaa kihisia na wanajua kuhusiana
vizuri na watu. Hii haina maana kwamba, kumwonesha mtu tabia hizo, kuna
maana ya kumpenda au kumpenda sana mwanamke. Dalili hizi ni nzuri na
inawezekana zikawa zinaonesha mwanaume kumpenda mwanamke, lakini
mwanamke asilichukulie jambo hilo kwa namna hiyo.
3. Mwanaume anaweza kuonesha kuwa na udadisi kuhusu mwanamke kwa maana
kwamba, kutaka kujua mambo yake, kumfuatilia au kuulizauliza kuhusu
habari za mwanamke. Hii haina maana kwamba mwanaume amempenda kimapenzi.
Inawezekana mwanaume akawa amevutiwa kimapenzi na mwanamke ndiyo maana
akaonesha tabia hizo, lakini siyo lazima iwe hivyo. Kumbuka kwamba,
mwanaume anaweza kuvutiwa na mazungumzo ya mwanamke, akavutiwa hata na
namna alivyo usoni, hivyo akapenda kuzungumza naye lakini siyo kwa
sababu anampenda.
4. Kuna wanaume ambao wana wake au wapenzi, lakini wanajisikia vizuri
kusikiliza wanawake wengine au kujua tu habari za wanawake wengine, bila
kuwa na haja ya kuanzisha uhusiano nao. Mwanaume anapompa mwanamke
‘ofa’ hasa ya chakula cha mchana au usiku, ni dalili ya wazi ya kuvutiwa
naye. Hapa kuna uhakika mkubwa zaidi, labda tu kama mazungumzo
yanayotajwa kufanywa wakati huo wa chakula yanafahamika, na ni ya
shughuli maalum. Kwa hiyo ‘ofa’ ya chakula ni dalili nzuri na yenye
uhakika. Lakini kuna jambo ambalo ni muhimu kwa mwanamke kulifahamu
katika hali kama hii. Kuna wakati mwanaume kumpa ‘ofa’ mwanamke kwa
chakula cha mchana au jioni, kunaweza kusiwe na maana ya moja kwa moja
kwamba, uhusiano utaundwa. Inawezekana katika kutoka outing huko, mwanaume akaghairi. Kwa wengine huchukua muda hadi kuamua kuhusu kuunda uhusiano au hapana.
5. Hata mwanaume kuamua kumpeleka mwanamke kwa familia yao na
kumtambulisha kama rafiki yake, ni hatua yenye kuonesha kwamba, mwanaume
ameamua kumpenda mwanamke huyo. Lakini wakati mwingine hii inaweza
ikawa ni janja yake kutaka tu kumthibitishia mwanamke ili amhadae
vizuri, na wala hakuna maana ya uhusiano wa kudumu.
6. Kuzungumza kwa pamoja kuhusu masuala ya baadaye ya kiuhusiano, kama
vile, idadi ya watoto na mambo mengine ambayo mara nyingi huzungumzwa na
watu ambao tayari wako kwenye uhusiano ni dalili ya mwanaume kuvutiwa
mwanamke. Lakini tatizo la jambo hili ni kwamba, kuzungumza masuala ya
baadaye inaweza kuwa ni njia ya mwanaume kutaka kujisikia au kujua jinsi
inavyokuwa katika mambo hayo. Inaweza kuwa pia ni njia yake ya kutaka
kupima wanawake wanavyosema kuhusu masuala hayo. Lakini inaweza ikawa
mwanaume huyo anatafuta kujua misimamo ya mwanamke huyo ili hatimaye
afanye uamuzi. Kwa hiyo, bado haioneshi kuwa amevutiwa na kuamua tayari.
Mara nyingi wanawake hudanganywa na dalili fulani zinazooneshwa na
wanaume wakati wanapoanza kuzoeana nao. Dalili hizi huwafanya kuamini
kwamba, wanaume hao wamewapenda tayari, wakati siyo kweli. Kwa kuangalia
baadhi ya dalili hizo kama nilivyozitaja, mwanamke anaweza kuwa makini
wakati anapoanzisha uhusiano, ili asikurupuke na kujikuta amedanganyika.
Ni kweli, kuna wakati ni dalili zinasema kweli, lakini kuna wakai
zinadanganya kuhusu kupenda au kupendwa.
KAMA UMEGUSWA NA HUDUMA ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.