Kucheka mara kwa
mara kutakuondolea msongo wa mawazo na mifadhaiko; pia kutakufanya
kulala usingizi mnono na kufurahia maisha yako. Uchekeshaji ni kitu
muhimu sana na ndio maana viongozi wakuu, waalimu na washauri nasaha
wengi ni wachekeshaji katika mazungumzo yao.
Mara nyingi
ninapozungumzia au kujadili kuhusu kucheka, huwa najiuliza, hivi ni ndoa
ngapi ambapo wanandoa wake hucheka na vicheko hivyo hutoka kwa wenzao?
Nalijua jibu, lakini silipendi, ingawa siwezi kuubadili ukweli. Kama
kuna ndoa kumi, basi ni ndoa mbili tu ambapo wanandoa wake hupeana afya
kupitia kuchekeshana.
Kwenye ndoa nyingi,
utakuta mke au mume amenuna muda wote. Hata mwenzake anapojaribu
kumchekesha ili kufanya hali iwe na mwelekeo wa amani na upendo, ni kazi
bure. Mke au mume huyu anapokuwa nje na nyumbani kwake, ni mchekaji
mzuri sana tena wa vichekesho vya kawaida mno!
Nimebaini kwamba, ndoa
inapokuwa na vichekesho yaani mzaha na utani usioumiza, humfanya kila
mwanandoa kutamani kuwa nyumbani kwake, humfanya kila mwanandoa kuhisi
haja ya ukaribu wa mwenzake. Lakini kubwa zaidi ni kwamba, mwanandoa
hujenga afya yake ya akili, mwili na hisia kupitia kicheko.
Mara nyingi nikitazama
zile sinema za dhati zilizobuniwa na wataalamu wanaojua Nyanja nyingi
za kimaisha, huwa ninaona kicheko kikitumiwa sana kuelezea au kuonesha
kama ndoa ni ya amani au vurugu. Kama ndoa ni ya amani, ni wazi utaona
wanandoa wakitaniana na kufurahia sana utani. Huu siyo ukweli wa
kisinema, bali ndio ukweli halisi.
Ndoa bora huweza
kupimwa kwa kiwango cha utani kati ya wanandoa. Hebu jaribu kufikiri kwa
hatua, halafu ujiulize, ni ndoa ngapi ngumu unazifahamu (pengine
ikiwemo yako). Halafu jiulize, huwa unakuta wanandoa hao wakitaniana
mara ngapi, kama imeshatokea ukawa karibu nao? Utapata jibu kirahisi
sana. Hujawahi, na kama umewahi, basi ni kwa tukio maalumu au tukio la
makusudi la wanandoa hao,kukuonesha wewe kwamba, wanandoa hao wako
katika amani.
Ukweli unaendelea
kubaki kwamba,kama wanandoa wanajua kuchekeshana, tena kwa makusudi,
vurugu ndogondogo huwa zinafutwa kirahisi sana. Ni lazima zifutwe kwa
sababu, hatimaye kila jambo huingizwa kwenye mzaha na kuvurugiwa humo.
Wataalamu wanasema, mahali popote ambapo watu wana dhati sana ya mambo (serious),
hapo kuna maumivu mengi. Kuna nyumba ambazo kila jambo linajadiliwa na
kuzungumzwa kwa sauti kavu na imara ya dhati – hakuna mzaha hata chembe.
Mke na mume wako pamoja tangu asubuhi, lakini hakuna hata mmoja ambaye
amemfanya mwenzake akacheka. Kama yupo anayejaribu , atakutana na
kizuizi cha, ‘si wakati wa mzaha huu.’
Napenda kukushauri
kwamba, hebu kuanzia hivi sasa anza kufanya mzaha mdogomdogo kwa
mwenzako, lakini wenye nguvu ya kuchekesha. Kama naye alikuwa hajui
utamu wa kuchekesha, ataujulia kwako na huenda naye akaanza kufanya
mzaha. Lakini mnaweza kwa pamoja kuamua kuanza kuyageuza maumivu mengi
kuwa mzaha na vichekesho. Hili linawezekana.
KAMA UMEGUSWA NA HUDUMA ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.