WAZIRI Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, amemtaka Rais Jakaya
Kikwete kusitisha mzunguko wa nne wa utoaji wa leseni za utafutaji wa
gesi asili na mafuta hadi sera na sheria ya gesi asili zikamilike, na
marekebisho ya sera ya nishati na sheria za mafuta yafanyike.
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo (CHADEMA), alisema hatua hiyo ni kurejea maoni na mapendekezo aliyoyawasilisha bungeni kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Mei 22 mwaka huu.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, alisema rais anapaswa kuchukua hatua hiyo kwa kuzingatia kwamba Mei 25 mwaka huu, badala ya kushughulikia mapendekezo hayo, Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo alitoa majibu ya uongo na upotoshaji bungeni kuhusu masuala mbalimbali.
“Aidha Ikulu inapaswa kueleza iwapo Baraza la Mawaziri chini ya Rais
Kikwete ndilo lililofanya uamuzi wa kuendelea na mchakato wa kutoa
leseni za vitalu vya utafutaji wa gesi asili bila ya kuwepo kwa sera ya
gesi asili na sheria ya gesi asili, na sera ya nishati na sheria
zinazohusu mafuta au ni maamuzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli
(TPDC) na Wizara ya Nishati na Madini,” alisema.
Mnyika aliongeza kuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda anapaswa kueleza
iwapo kauli ya kejeli, dharau na uongo ya hivi karibuni iliyotolewa na
Waziri Muhongo, kwamba uwezo wa wafanyabiashara wa Tanzania ni kuwekeza
kwenye soda na juisi, si kwenye sekta ya gesi, ni msimamo wa serikali au
maoni ya waziri binafsi.
“Izingatiwe kwamba Wizara ya Nishati na Madini, kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), imetangaza mzunguko wa nne wa utoaji leseni za utafiti wa gesi asili na mafuta katika vitalu nane ndani na nje ya maji ya Ziwa Tanganyika vyenye ukubwa wa kilomita za mraba elfu tatu kila kimoja utakaofanyika Oktoba 2013.
“Serikali pia imetenga mipaka ya vitalu viwili kwenye bahari kuu, na kuingia ubia wa utafiti na kampuni inayoitwa mbia wa kimkakati (Strategic Partner) ambae serikali haijamtaja,” alisema.
Alisema mchakato huu unafanyika wakati taifa likiwa halina sera (mchakato wa kuiandika bado unaendelea) na hatimaye yaanze maandalizi ya kupata sheria mahususi za kusimamia sekta ndogo ya gesi, hatua ambayo inapaswa kuambatana na marekebisho ya kisera na kisheria ya sekta.
Aliongeza kuwa tayari Tanzania imeshafanya ugunduzi wa futi za ujazo zaidi ya trilioni 32 za gesi katika maeneo kadhaa nchini, hivyo kuifanya kuwa kati ya nchi vinara wa gesi nyingi Afrika na duniani.
“Utajiri huu wa gesi hadi sasa hauna sera wala sheria zinazotoa mwongozo wa usimamizi na udhibiti wake, ili kuhakikisha unawanufaisha Watanzania, kuepuka makosa yaliyofanyika katika uwekezaji mwingine wa gesi asili na rasilimali nyingine uliofanyika bila mifumo thabiti,” alisema.
KAMA UMEGUSWA NA HUDUMA ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.