MWANAFUNZI wa darasa la sita, Ismail Godfrey (13) anayesoma katika
Shule ya Msingi Maendeleo Sinuka iliyopo mkoani Kigoma amejikuta kwenye
wakati mgumu baada ya kudai kutandikwa viboko na Mwalimu Muige Joseph
na kupooza miguu.
Mtoto huyo ambaye kwa sasa anapata matibabu katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili jijini Dar baada ya kukosa matibabu ya kina mkoani Kigoma
alipokutana na mwandishi wetu alikuwa na haya ya kusema:
“Awali sikuwa na matatizo yoyote ya kiafya hususan katika viungo vya
mwili, isipokuwa haya yalinipata baada ya kuchapwa fimbo na mwalimu
wangu ndipo nikapooza ghafla.
Miguu ya mtoto Ismail iliyopooza.
“Tukio hili lilitokea mwezi wa tano nilipokuwa shuleni, nilipofika
nilifungua bomba nikawa nakunywa maji kwa kuwa nilikuwa na kiu, ghafla
mwalimu huyo alikuja na kuniambia kwa nini nachezea boma, ndipo akaanza
kunitandika viboko.
“Hapo hapo nikahisi viungo vyote vya mwili vimepoa na miguu ikapata
ganzi, nikaanguka chini baada ya kukosa nguvu,” alisema Ismail.
Kutokana na tukio hilo baba wa mtoto huyo, Godfrey Lucas aliitwa na
baada ya kuona Ismail yupo katika hali hiyo ya kupooza miguu aliamua
kumpeleka katika Hospitali ya Mkoa, Maweni, kupatiwa matibabu, huku
akifanya juhudi za kumtafuta mtuhumiwa ambaye alikuwa amekimbia makazi
yake.
Ismail Godfrey.
Hata hivyo , kutokana na juhudi za kumtafuta kwa kushirikiana na
wananchi walifanikiwa kumkamata mwalimu huyo katikati ya mji wa Kigoma
na kumfikisha polisi ambapo alifunguliwa kesi kwa jalada namba
KIGO/RB/2269/013 17/3/2013 SHAMBULIO LA MWILI.
“Mtoto alianza kutokwa na vidonda miguuni ndipo nikaamua tuje hapa
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na tukapokelewa na mtoto amelazwa
wodi ya wagonjwa ya Kibasila,” alisema.
Hata hivyo, amesikitika kuachiwa mtuhumiwa kwa dhamana wakati mwanaye bado kalazwa na anakosa masomo kwa sababu yake.
KAMA UMEGUSWA NA HUDUMA ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.